Kumbukumbu Uholanzi na visa ya Schengen

 

Ufanye nini unapokuwa na saa 24 tu za kutalii katika nchi Fulani?hata mimi sifahamu,lakini ngoja nikusimulie kisa changu,pengine utapata cha kufanya.

Mwaka 2023,nilipata ufadhili wa masomo ya muda mfupi nchini Uholanzi,ufadhili huo uligharamia safari ya kwenda na kurudi ,malazi na chakula cha asubuhi na mchana,huku tukilipwa yuro kumi kwa ajili ya chakula cha jioni kila siku.Ukweli ni kwamba ilikuwa mara yangu ya kwanza Kwenda bara la Ulaya,nilikuwa na furaha na shauku kubwa sana.Wakati nikijiandaa na safari,nilifanya utafiti na kugundua kuwa,nchi ya Uholanzi ni miongoni mwa nchi mwanachama wa eneo la Schengen,na kwa kupata visa ile nilikuwa na uwezo wa kutembelea takribani nchi 20 zaidi kwa kutumia visa ile moja,nilifurahi sana.

Safari ya kutoka Dsm mpaka Amsterdam ilikuwa safari nzuri sana,iliyojaa hamu na ghamu,haswa ikizingatiwa kwamba nilikuwa nasafiri wakati ya ,majira ya Baridi(huko niendako)na nikitoka katika majira ya joto kali nchini mwangu.

Kwenye ndege kutoka Tanzania mpaka Nairobi,nilikaa jirani na mtu tuliyefahamina,safari ya saa moja na nusu ilikuwa fupi kama mkia wa mbuzi,kufumba na kufumbua tulikuwa tumefika Nairobi.Tuliendelea na gumzo hapa na pale kisha kila mtu akaelekea katika geti lake la safari,mwenzangu alikuwa akielekea nchini Afrika Kusini kikazi ,huku nami nikielekea nchini Uholanzi,kimasomo(kwa masomo ya utaalamu ya majuma matatu).

Safari ya kutoka Nairobi mpaka Amsterdam,ilichukua takribani saa nane hivi.Tulitoka Nairobi saa mbili Asubuhi na kufika uholanzi saa 10 na nusu Jioni.Baada ya kuwasili,ndege ilitushusha eneo mbalo tulilazimika kutembea takribani kilometa moja ndani ya uwanja kabla ya kufika sehemu ya kuchukua mizigo na kisha kutoka nje ya eneo la Uwanja wa ndege ambapo wenyeji wetu walikuwa wakitungojea ili kutupokea.

Afaanaleki!Baada ya kutoka nje ya uwanja,tulikutana na baridi kali na kulazimika kufungua -begi na kutoa nguo za baridi ambazo tuliambiwa tubebe(tulitumiwa maelekezo ya nguo za kubeba).Nilitoa boshori,nguo yenye urefu wa kufunika mpaka shingo,na koti refu ,na baada ya kutoka nje kabisa,nilipigwa na baridi kali sana usoni na kulazimika kutoa barakoa ili kukabiliana na hali ile.

Safari kutoka Uwanja wa ndege wa Schipol Amsterdam,kuelekea Haarlem ikawaida.Uwanjani tulipokelewa na bi Hillary,ambaye alikuwa anahusika na mapokezi ya watu wapya,tukajikuta watu 6 pamoja,m-Zambia mmoja,wa Misri watatu,Mtanzania mimi,Tukapatiwa kadi za kupandia basi ambazo zilikuwa zinaisha muda kwa siku hiyo saa tano usiku.Tukapandishwa gari ,isivyo bahati lilikuwa likienda uelekeo tofauti na mahali tulipaswa Kwenda,baada ya mwendo wa takribani nusu saa,tukashuka,halafu tukapanda gari jingine lililoelekea mahali tulipaswa Kwenda,na kufanya safari kuchukua saa nzima huku basi likipita tena maeneo ya uwanjani,tulikasirika sana na hatukuwa na la kufanya,baada ya mwendo wa  saa moja na nusu,tulifika na kushuka katika kituo Jirani na hoteli ya Niu Diary,mahali tulipotakiwa kuishi kwa majuma matatu ya mafunzo yetu.

Tulifikaje hotelini?Bada ya kushuka,tulianza kuuliza watu kwa kiingereza ambapo wengi wao hawakukifahamu,tukiwaonesha jina la hoteli kwenye karatasi zetu,na bado kushindwa kupata msaada,na baada ya kushangaa na kuelekea mwelekeo mwingine mbali kabisa na hoteli ilipokuwa,bahati ilikuwa upande wetu,tukakutana na wanawake wawili Weusi(baadaye tukafahamu wanatoka Nigeria)ambao kwa kutuona tu na mabegi yetu,walifahamu tunapoelekea na wakatuambia kozi tuliyokuwa tumeifuata,na kutuambia tuwafuate na  tukawafuata.(Wale wa Misri hawashuka Nasi,hivyo walienda mpaka mwisho wa gari na baada ya saa moja wakarejea tulipo.)

Mji wa Haarlem,ni mji wa zamani,wenye majengo ya kizamani,na mitaa mchanganyiko lakini ukiwa na utajiri wa historia,ikiwemo kanisa kubwa lililojengwa miaka ya 1700,town hall,eneo la kusanyiko na makumbusho kadha wa kadhaa,huku kukiwa na maduka ya jibini Pamoja na bar zinaouza bangi.Ndiyo,Bangi!Ilikuwa ajabu kuona lakini ndiyo moja ya alama ya Uholanzi,kwao bangi ni bidhaa tu  na  inauzwa bila kificho.



 Kutoka hotelini mpaka shuleni,ilikuwa ni sehemu ya umbali wa takribani dakika 30 kwa mwendo wa haraka ,na dakika 40 kwa mwendo wa pole,siku ya kwanza tuliona mateso,lakini baada ya kuita uber na kuona gharama ya kufika shuleni ni Yuro 10,tukawa wapole na kuamua kujfuata utaratibu wa kutembea(hata hivyo ilikuwa baridi sana,kutembea ilikuwa ni vyema zaidi).

Juma la kwanza likaisha,kutahamaki,hatujaenda popote,kundi la waindonesia walienda Ujerumani kutalii,nasi tukakumbuka kwamba,zaidi ya safari ya shuleni na kurejea hatukufanya utalii wowote ule,tukaamua jumapili Asubuhi Kwenda The Hague,mji wa kiserikali wa Uholanzi.Safari ya watu 5 ikaanza,wa Tanzania 2,m Congodrc 1,Ethiopia mmoja,na m Yemen mmoja.Majira ya saa tano asuhuhi jumapili,tukatoka kuelekea kituo cha mabasi na metro cha Haarlem terminus.

Baada ya dakika 45 za kutembea tukafika kituoni,na baada ya kufaya hesabu tukaona njia salama ni kununua kadi ya metro ili kurahisisha usafiri na kuokoa fedha,ambapo kila mtu alinunua kadi kwa yuro 50,yuro 20 kama malipo ya kadi na yuro 30 za matumizi.

Safari ya kuelekea Hague ikaanza,na baada ya dakika 45 na kubadili treni mara moja,tukafika katika kituo kikuu cha treni cha Hague,tukamsubiri rafiki wa m Yemen ambaye alisema angekuja kutupokea na kisha tukaanza kutembea nje ya kituo.Mji wa Hague,ulikuwa na majengo makubwa Pamoja na bendera mbalimbali za mataifa mengi katika baadhi ya sehemu,kuashiria kuwa mji huo ni wa kimataifa.Tulitembea katika mitaa ambayo ilikuwa imechangamka kwa mikahawa na bar zenye nakshi tofauti tofauti.

Baada ya kuzunguka takribani saa nzima,tukaamua sasa tunataka kuiona mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai,ICC na hapo tukaagana na mwenzetu wa ki Yemen Pamoja na rafiki yake,kisha sisi wanne tukapanda uber mpaka ICC ama kwa jina maarufu the HAGUE.Dereva wetu alikuwa m Pakistan,ambaye alitupa hadithi nyingi za kuchekesha lakini haswa akisema anaifahamu Tanzania maana alishafanya kazi katika kiwanda cha nguo.kueleka hague,mji ulipoa sana hasw ikizingatiwa ilikuwa mwisho wa juma na ni eneo la kisreikali zaidi,tulipokewa na ukimya mkubwa Pamoja na hali ya mawingu na baridi kali.

Tulishuka baada ya kufika Hague,na kusogelea mpaka geti la kuingia ambapo kuna machine ambayo tuliiuuliza utaratibu na ikatuambia tunaweza kupiga picha nje tu maana siku hiyo haikuwa ya kutembelea.

Tulipiga picha nyingi na kufurahi nje ya jengo hilo,ikiwemo Mabawa maarufu ya msanii wa Mexico ambayo yako sehemu mbalimbali duniani ikiwemo hapo,na kisha tukahitimisha safari yetu katika mji wa Hague kwa kupanda daladala mpaka kituo kikuu cha treni kwa safari ya kurejea Haarlem ambapo mbele ya safari uelekeo ukabadilika na kuwa Amsterdam!

Itaendelea…………..

 

Comments

Popular posts from this blog

Mafia Island,hidden paradise of Tanzania!

Meeting in the bush!